SERIKALI
inatarajiwa kutoa utaratibu wa namna wanafunzi wa shule za Serikali za
mabweni, watakavyosoma huku ikionya wakuu wa shule watakaodai ada au
michango ya aina yoyote, kwamba watachukuliwa hatua ikiwemo kufukuzwa
kazi.
Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Jumanne Sagini amesema hayo jana wakati akifungua Mkutano
Mkuu wa Kitaifa wa mwaka wa wadau wa Camfed unaofanyika mjini hapa.
Katika
hotuba yake iliyosomwa na Mkurugenzi Idara ya Usimamizi wa Elimu,
Benard Makali, Sagini alisema kuanzia Januari 2016, elimu nchini katika
shule za msingi na sekondari itatolewa bure.
Alisema
shule zenye hosteli kisheria, usajili wake ni shule za kutwa na
zitapewa utaratibu wake katika uendeshaji na Serikali itakaa na kutoa
maelekezo sahihi ili wazazi wasaidie kuchangia chakula.
Amesema Serikali itakaa na kutoa maelekezo sahihi, ili wazazi wasaidie mipango mizuri ya halmashauri.
“Chakula
si pesa kama wazazi watakubaliana kuchangia chakula wakati wa mavuno
hiyo itakuwa sawa lakini serikali itatoa maelekezo,” alisema.
Alisema
kila halmashauri inaweza kuwa na utaratibu wake juu ya suala hilo.
Alisema shule hizo wanafunzi wake hawatalipa ada wala michango yoyote
lakini wazazi watalazimika kuwanunulia wanafunzi sare, madaftari na
usafiri wa kuwapeleka na kuwarudisha nyumbani wakati wa likizo.
Makali alisema awali wanafunzi walikuwa wakilipa ada ya Sh 70,000 kwa mwaka lakini hawatalipa tena ada wala michango yoyote.
“Taratibu zimeshafanywa na shule zitafunguliwa kwa wakati na hakuna mwanafunzi atakayelipa ada au mchango wa aina yoyote” alisema.
Alipohojiwa
ni kwa jinsi gani huduma katika shule za bweni zitaboreshwa ikiwemo
kuwalipa wapishi na walinzi ambao kwenye maeneo mengi hawajaajiriwa na
serikali, Mkurugenzi huyo alisema masuala yote yatatolewa ufafanuzi.
Akizungumzia tatizo la utoro limekuwa likirudisha nyuma maendeleo ya watoto wengi.
“Ukimuuliza Ofisa Wilaya anasema mwamko mdogo wa wazazi, hivi hao wazazi wanaowasingizia siku zote wako nchi nzima?" Alisema. Aliwataka maofisa elimu kufanya kazi zao na si kuwasingizia wazazi.
“Tunapoteza
watoto wengi, wanazurura tu sioni kwa nini suala hili linaendelea,
mtoto asipoonekana shuleni mwalimu asikae kimya,” alisema.
Alisema
sasa watachukua hatua kali kwa walimu atakaozembea suala la utoro kwa
wanafunzi. Pia alilipongeza shirika hilo kwa kusomesha watoto wa kike
walio katika mazingira magumu na kuwa serikali itaunga mkono juhudi
hizo.
Awali, Mkurugenzi wa Camfed Tanzania, Lydia Wilbard alisema watoto 48,373 wameweza kufikiwa na shirika hilo.
0 comments:
POST A COMMENT